EVENT DESCRIPTION
Tumsifu Yesu Kristo. Taarifa hii inatolewa na Idara ya Elimu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kuhusu matokeo ya mtihani wa kidato cha nne wa mwaka 2024 kwa shule za Kanisa Katoliki.
Lengo la kutolewa kwa taarifa hii ni kutoa tathmini ya ufaulu wa shule hizo ili kubaini maendeleo ya kitaaluma, maeneo yanayohitaji maboresho, na mwelekeo wa jumla wa elimu katika taasisi hizo.
Kwa mujibu wa takwimu, jumla ya watahiniwa wote nchini Tanzania walikuwa 516,695. Kati yao, wanafunzi wa shule za Kanisa Katoliki walikuwa 19,182, sawa na asilimia 3.6 ya watahiniwa wote.
Kwa upande wa ufaulu, wanafunzi waliopata daraja la kwanza hadi la tatu walifikia 18,745, sawa na asilimia 97.72 ya watahiniwa wa shule za Kanisa. Wanafunzi waliopata daraja la nne walikuwa 128 (asilimia 2.23), huku waliopata daraja la sifuri wakiwa watu 9 tu, sawa na asilimia 0.04.
Ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2023, ufaulu wa shule za Kanisa umeendelea kuimarika. Mwaka huu, kiwango cha ufaulu kimeongezeka kwa asilimia 1.66, tofauti na ongezeko la asilimia 0.15 mwaka uliotangulia.
